Rahmani Fazli: Vita dhidi ya mihadarati vinahitajia ushirikiano wa kieneo na kimataifa
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kuwa mapambano dhidi ya madawa ya kulevya yanahitajia ushirikiano wa kieneo na kimataifa.
Abdolreza Rahmani Fazli Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema leo katika Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Madawa ya Kulevya hapa Tehran kuwa Iran imeandaa nyanja zinazohitajika ili kushirikiana kiintelijinsia na kioparesheni kwa kutumia mifumo ya kieneo na kimataifa katika mapambano dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya, hata hivyo amesema aina hii ya ushirikiano unapasa kuwa makini zaidi na unaokwenda sambamba na wakati unaohitajika kutoka nchi nyingine.
Rahmani Fazli ameongeza kuwa Iran ikiwa ni nchi ya kwanza katika njia ya Balkan, ni ya kwanza kukabiliwa na mawimbi makubwa ya magenge ya magendo ya mihadarati na jinai nyingine. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni nchi inayoongoza mapambano dhidi ya madawa ya kulevya duniani, hadi sasa imepoteza mashahidi zaidi ya 3500 na wananchi wake wengine zaidi ya 10,000 wamejeruhiwa katika mapambano hayo. Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Magendo ya Madawa ya Kulevya umeanza leo hapa Tehran lengo likiwa ni kuchunguza mchakato wa magendo ya mihadarati kuanzia njia ya Balkan na pia njia za ushirikiano dhidi ya magendo hayo na jinai nyingine zilizoratibiwa.