Qassemi: Iran inalaaani matumizi ya aina yoyote ya silaha za kemikali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran inalaani matumizi ya aina yoyote ya silaha za kemikali bila ya kujali waliofanya na aina ya wahanga wa mashambulio hayo.
Zaidi ya watu 100 wameuawa na karibu 400 kujeruhiwa katika shambulio la jana la silaha za kemikali kwenye eneo la Khan Shaykhun, kusini mwa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. Hivi sasa eneo hilo liko mikononi mwa magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi na Uturuki. Magaidi hao wamekimbilia Idlib baada ya kupata pigo kubwa na kufurushwa katika mji wa kiistratijia wa Halab (Aleppo).
Komandi Kuu ya jeshi la Syria imekanusha vikali madai ya maadui wa Syria wanaolihusisha jeshi hilo na shambulio hilo na kusisitiza kuwa, magenge ya kigaidi ndiyo yaliyofanya shambulizi la kemikali huko Idlib hiyo jana.
Mwandishi wa IRIB amemnukuu Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema leo kuwa, hii si mara ya kwanza kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria na hadi hivi sasa pande zenye maslahi yao haramu nchini Syria zimekuwa zikikwamisha juhudi za kukomesha kikamilifu mashambulizi hayo.
Amesema, lengo la mashambulizi hayo ya kikatili nchini Syria ni kukwamisha na kuvuruga juhudi za kisiasa za kuutafutiwa ufumbuzi mgogoro wa miaka sita sasa wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesema, kwa kuzingatia historia ya magenge ya kigaidi nchini Syria ya kumiliki na kujilimbikizia silaha za kemikali, Tehran inaamini kuwa, kutopewa umuhimu suala la kuyapokonya silaha za kemikali magenge hayo ni tatizo kubwa nchini humo.