Iran kuanza kuunda ndege kubwa za abiria
(last modified Sat, 15 Apr 2017 14:04:52 GMT )
Apr 15, 2017 14:04 UTC
  • Iran kuanza kuunda ndege kubwa za abiria

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema, mafanikio ya nchi hii katika kuunda ndege ya kivita ya Qaher 313 na kutoa mafunzo ya Kauthar 88 ni utangulizi wa Iran kuunda ndege kubwa za abiria na mizigo.

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan ameyasema hayo leo mjini Tehran pembizoni mwa uzinduzi wa mafanikio mapya katika sekta ya ulinzi wa Iran hasa uundwaji ndege ya kivita ya Qaher 313 na ya kutoa mafunzo ya Kauthar 88.  Dehqan amesema kuwa Qaher 313 ni ndege ambayo haijatengenezwa kwa kutumia chuma bali ni kwa mada za composite. Aidha ameongeza kuwa, kati ya mafanikio yaliyozinduliwa leo ni pamoja na drone au ndege isiyo na rubaini aina ya Muhajir 6 ambayo ni ya kizazi kipya.

Ndege ya kivita ya Qaher 313 iliyoundwa nchini Iran

Brigedia Jenerali Dehqan amesema katika maonyesho hayo ya mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran kumezinduliwa helikopta aina ya Saba 248 na kifaru cha Karrar na kusema: "Zana hizi mbili za kujihami ni kati ya mafanikio makubwa ya Wizara ya Ulinzi ya Iran na zimetegenezwa kikamilifu kwa kutegemea uwezo wa wataalamu wa hapa nchini. 

Maonyesho hayo ya mafanikio ya Wizara ya Ulinzi ya Iran yamefunguliwa Jumamosi hii katika sherehe iliyohudhuriwa na Rais Hassan Rouhani.