Kikao cha wataalamu wa amani ya Syria chaanza mjini Tehran
Kikao cha wataalamu wa masuala ya amani na utulivu wa Syria ambacho ni muendelezo wa mazungumzo ya amani ya Astana Kazakhstan, kimeanza leo Jumanne hapa mjini Tehran.
Ajenda kuu ya kikao hicho ni kujadili njia za kuimarisha makubaliano ya kusimamisha vita na kinawashirikisha wataalamu kutoka Iran, Russia, Uturuki na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo ya amani ya Syria hadi sasa yameshafanyika mara tatu huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan na kuhudhuriwa na nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki ambao ni waitishaji wakuu wa mazungumzo hayo yanayowashirikisha pia wajumbe kutoka serikali ya Syria na makundi yenye silaha pamoja na Stephen De Mistura, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Syria.
Imetangazwa kuwa, kikao cha nne cha mazungumzo ya amani ya Syria kitafanyika tarehe tatu na nne Mei 2017 huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan.
Wakati huo huo Alauddin Burujerdi, mkuu wa kamisheni ya usalama wa taifa na siasa za nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amesema, kuna ulazima kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha kujadili na kuchunguza jinai zilizofanywa na magaidi dhidi ya raia wa Syria huko magharibi mwa mkoa wa Halab, magharibi mwa Syria..