Marekani inajaribu kuvuruga ushirikiano wa Iran na benki za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28448-marekani_inajaribu_kuvuruga_ushirikiano_wa_iran_na_benki_za_kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameilaani vikali serikali ya Marekani kwa kujaribu kuvuruga miamala baina ya Iran na mfumo wa kimataifa wa benki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 30, 2017 03:11 UTC
  • Marekani inajaribu kuvuruga ushirikiano wa Iran na benki za kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameilaani vikali serikali ya Marekani kwa kujaribu kuvuruga miamala baina ya Iran na mfumo wa kimataifa wa benki.

Akihutubu katika Mkutano wa 4 wa Benki na Biashara baina ya Iran na Ulaya mjini Tehran, Zarif amesema  vikwazo ambavyo mfumo wa benki wa Iran uliwekewa kabla ya kufukiwa mapatano ya nyuklia na kundi la 5+1 vililenga kulemaza mfumo wa kifedha na kibenki nchini Iran.

Zarif amesema Marekani inatoza faini kubwa kwa benki za kimataifa ambazo zinafanya kazi na Iran kwa kisingizio cha vikwazo. Amebainisha masikitiko yake kuwa,  matamshi ya wakuu wa serikali mpya ya Marekani yamepelekea mfumo wa benki za kimataifa kuchukua tahadhari sana katika kufanya kazi na Iran.

Zarif pia ameituhumu Marekani kwa kufuata sera za ujambazi kufuatia hatua yake ya kuchukua kwa nguvu udhibiti wa mali za Iran katika benki za kimataifa. Amesema mfano wa wazi wa ujambazi huo wa Marekani ni kudhibiti kwa mabavu dola bilioni 2 na pia mali zenye thamani ya dola bilioni 1.5 ambazo ni milki ya Benki Kuu ya Iran.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.

Hata hivyo Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 5+1 inakwepa kutekeleza ahadi zake na badala yake imekuwa ikichukua hatua ambazo zinakiuka makubaliano hayo ya nyuklia.