Rais Rouhani atoa mkono wa pole kwa familia za waliofia mgodini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28632-rais_rouhani_atoa_mkono_wa_pole_kwa_familia_za_waliofia_mgodini_iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali iliyotokea mgodini kaskazini mashariki mwa nchi hapo jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2017 03:11 UTC
  • Rais Rouhani atoa mkono wa pole kwa familia za waliofia mgodini Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali iliyotokea mgodini kaskazini mashariki mwa nchi hapo jana.

Sanjari na kutoa mkono wa pole kwa familia za waliofariki dunia huku akiwatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa katika ajali hiyo, Rais Rouhani amezitaka mamlaka zote husika kuishughulikia kwa uzito kadhi hiyo hususan utoaji wa misaada yote inayohitajika ikiwemo ya kutibiwa majeruhi na mipango ya mazishi kwa waliopoteza maisha katika mkasa huo.

Hapo jana Dakta Rouhani aliwaagiza Waziri wa Viwanda na Maadini pamoja na mwenzake wa Ushirika na Wafanyakazi wa Iran kwenda mkoani Golestan kutathmini hali kwa karibu na kusimamia shughuli za kuokolewa na kutibiwa majeruhi wa mkasa huo.

Shughuli za kuwaokoa majeruhi wa mkasa wa Golestan

Mkurugenzi wa Shirika la Kushughulikia Majanga hapa Iran amesema waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea katika mgodi wa makaa ya mawe wa Azadshahr ulioko mkoani Golestan, kaskazini mashariki mwa nchi, ni wachimba migodi 21 na kwamba wengine 49 wamejeruhiwa.

Siku tatu za maombolezo zimetangazwa katika mkoa wa Golestan. Mgodi wa makaa ya mawe wa Azadshahr, mkoani Golestan una takriban wachimba migodi 500.