Ripoti ya Ahmad Shahidi; ni ripoti yenye malengo ya kisiasa
Ahmad Shahid Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amekariri tena ripoti yake ya kila mwaka kuhusu Iran.
Ripoti hiyo ambayo imeakisiwa na baadhi ya duru za habari, imejumuisha matamshi na tuhuma zisiso na msingi, ambazo Ahmad Shahid ametumia kama kisingizio cha kuchafua tasiwira ya Iran.
Katika ripoti hiyo pia kama ilivyokuwa huko nyuma, Ahmad Shahid amejaribu kila awezalo kuzibainishia nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu wasiwasi uliopo kuhusu haki za binadamu nchini Iran. Ripoti hiyo inatarajiwa kupigiwa kura katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva karibu wiki mbili zijazo.
Ripoti ya Alhamisi ya Ahmad Shahid Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Haki za Binadamu imedai kuwa mamia ya waandishi habari, wanaharakati na wapinzani wa serikali nchini Iran wamefungwa jela.
Kukosolewa utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu wanaojihusisha na biashara ya mihadarati, ni moja ya masuala yaliyoashiriwa kwenye ripoti hiyo. Ahmad Shahid ameitaka Iran iache kutoa hukumu za kifo kwa jinai zinaohusiana na madawa ya kulevya.
Hii ni katika hali ambayo aghalabu ya vitendo hivyo huhesabiwa kuwa ni jinai kwa mujibu wa sheria za Kiislamu na hukumu zinazotolewa kwa jinai hizo ni adhabu ya kifo. Huenda kwa mtazamo wa Ahmad Shahid suala hilo si jinai; hata hivyo swali linaloulizwa hapa ni hili kuwa je, wahalifu ambao waziwazi wanakusudia kuiangamiza jamii wanapasa kuadhibiwa vipi? Katika nyanja nyinginezo yapo maswali na shaka nyingi kuhusu malengo yaliyokusudiwa kwenye ripoti hiyo ya upande mmoja ya Ahmad Shahid. Kwa mfano swali hili linaulizwa kuwa je, kukandamizwa maandamano na malalamiko ya wananchi na vile vile ukandamizaji unaofanywa dhidi ya raia weusi nchini Marekani au miamala inayotekelezwa na serikali ya Uingereza na Ufaransa, Canada na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya kuhusu ubaguzi, haiwezi kufuatiliwa na kuchunguzwa kwa vigezo vya haki za binadamu za nchi za Magharibi?
Ni wazi kuwa Ahmad Shahid ameashiria suala la haki za binadamu katika ripoti yake hiyo kwa malengo ya kisiasa moja kwa moja kwa kupuuza vigezo vya kimaadili na thamani za kiutamaduni na kidini za nchini Iran, badala ya kuzingatia uhakika wa mambo kuhusu haki za binadamu. Ripota Maalumu wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia pia kuhusu ubaguzi dhidi ya wanawake, jamii ya walio wachache na haki ya uhuru wa kusema na kutoa maoni kwa mtazamo wake huo wa uwongo na wa upande mmoja. Ripoti hiyo vile vile imeashiria kuhusu uchaguzi na kukosoa namna Baraza la Kulinda Katiba lilivyoainisha ustahiki wa wagombea wa uchaguzi.
Ukweli ni kuwa ripoti hiii ni muendelezo wa ripoti za huko nyuma za Ahmad Shahid, ambayo imetathmini hali ya haki za binadamu nchini Iran kwa kushauriwa na nchi kama Canada, Marekani na Uingereza.
Ripoti hii imetolewa wakati huu ambapo nchi za Magharibi zimeanzisha harakati mpya za kujaribu kuchafua jina la Iran baada ya mpango wa JCPOA. Madai ya kutiwa wasiwasi na uwezo wa kimakombora wa Iran na madai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi, ni moja ya masuala yaliyoelekezwa kwa Iran ndani ya ripoti hiyo. Hakuna shaka kwamba ripoti kama hizo zinatolewa katika fremu ya mashinikizo ya Magharibi dhidi ya Iran; huku miamala ya undumakuwili kuhusu haki za binadamu ikishuhudiwa katika ripoti hiyo.