Uchaguzi wa Rais wa Iran kufanyika katika nchi 102 duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29258-uchaguzi_wa_rais_wa_iran_kufanyika_katika_nchi_102_duniani
Mkuu wa kamati ya kusimamia uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi amesema kuwa, uchaguzi huo utafanyika katika nchi 102 na kwenye vituo 310 katika nchi mbalimbali duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2017 10:56 UTC
  • Hassan Qashqavi, Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya bunge na balozi za Iran nje ya nchi
    Hassan Qashqavi, Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya bunge na balozi za Iran nje ya nchi

Mkuu wa kamati ya kusimamia uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi amesema kuwa, uchaguzi huo utafanyika katika nchi 102 na kwenye vituo 310 katika nchi mbalimbali duniani.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Hassan Qashqavi akisema hayo leo na kuongeza kuwa, vituo 55 vya kupigia kura vitawekwa nchini Marekani, 21 nchini Imarati, 22 nchini Iraq na 12 nchini Uingereza. 

Amesema, kulikuwa kumefanyika mazungumzo ya kuhakikisha raia wa Iran walioko nchini Canada nao wanapiga kura ndani ya nchi hiyo, lakini mazungumzo hayakufanikiwa, hivyo kumewekwa vituo vya kupigia kura katika mpaka wa Marekani na Canada ili raia wa Iran wanaoishi Canada nao waweze kutumia haki yao ya kuchagua rais wanayemtaka.

Wagombea wa uchaguzi wa 12 wa Rais wa Iran. Wawili wamejiondoa katika kinyangányiro hicho kwa maslahi ya wagombea wawili. Waliojiondoa ni Es'haq Jahangiri kwa maslahi ya Hassan Rouhani na Mohammad Baqer Qalibaf kwa maslahi ya Sayyid Ibrahim Raeisi

 

Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya bunge na balozi za Iran nje ya nchi amegusia pia namna raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi walivyolipokea vizuri suala hilo na kusema kuwa, hatua za lazima zimechukuliwa ili kusimamia vizuri uchaguzi huo. Amesema, katika kila nchi uchaguzi huo utaanza kufanyika saa mbili asubuhi kwa saa za eneo husika na utaendelea hadi za 12 jioni. Hata hivyo mabalozi na wawakilishi wa Iran katika nchi hizo wataweza kuongeza muda huo wa kupiga kura kama italazimu kufanya hivyo.

Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).