Uchaguzi; hamasa nyengine ya kihistoria iliyoonyeshwa na wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29292-uchaguzi_hamasa_nyengine_ya_kihistoria_iliyoonyeshwa_na_wananchi_wa_iran
Uchaguzi wa 12 wa rais, uchaguzi wa tano wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji na uchaguzi mdogo wa bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilifanyika kuanzia saa mbili asubuhi ya leo Ijumaa katika vituo 63,500 vya upigaji kura nchini kote.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
May 19, 2017 10:14 UTC
  • Uchaguzi; hamasa nyengine ya kihistoria iliyoonyeshwa na wananchi wa Iran

Uchaguzi wa 12 wa rais, uchaguzi wa tano wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji na uchaguzi mdogo wa bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilifanyika kuanzia saa mbili asubuhi ya leo Ijumaa katika vituo 63,500 vya upigaji kura nchini kote.

Sambamba na hapa nchini, Wairani waishio nje ya nchi, nao pia walifika kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais. Upigaji kura nje ya nchi umefanyika kwenye nchi 102 katika vituo 310 vya upigaji kura.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa miongoni mwa waliopiga kura zao mara baada ya zoezi la uchaguzi kuanza

Wairani 56,410,234 waliokuwa wametimiza masharti ya kupiga kura leo walimiminika kwenye vituo mbalimbali kutumbukiza kura zao katika masanduku ya kupigia kura za chaguzi zilizofanyika nchini. Mara baada ya kufunguliwa vituo vya kupigia kura saa mbili asubuhi ya leo, wananchi wa matabaka mbalimbali walianza kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kushiriki kwa hamasa katika zoezi hilo linaloonyesha jinsi taifa la Iran lilivyojiandaa kusajili kumbukumbu nyengine ya historia ya kujivunia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kumiminika kwa wingi wananchi katika vituo vya kupigia kura kumeonyesha jinsi wananchi hao wanavyoupa umuhimu mustakabali wao na wa nchi yao kupitia uchaguzi wa 35 kufanyika hapa nchini Iran tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Spika wa Bunge Ali Larijani akipiga kura

Taathira ya mchango wa wananchi katika chaguzi 34 zilizopita imezidisha msisimko wa kisiasa na uathirifu wao katika uchaguzi wa leo. Kwa mara nyengine tena, leo Iran ya Kiislamu imeudhihirishia ulimwengu maana halisi ya ushirikishi wa kisiasa wa umma. Ushirikishi wa kisiasa nchini Iran unadhihirika kupitia upigaji kura wa moja kwa moja wa wananchi kumchagua rais, ambaye ni kiongozi wa pili wa ngazi ya juu kabisa baada ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Rouhani (kushoto) na Sayyid Ibrahim Raisi, wagombea wakuu wa uchaguzi wa rais

Ushirikishi huo wa kisiasa, mbali na kuonyesha jinsi wananchi walivyofungamana na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kupita miaka 39 tangu kuasisiwa kwake, unaongeza na kuimarisha pia nguvu na usalama wa taifa la Iran. Mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi ambao unatawala hapa nchini, unaupa umuhimu maalumu mchango na nafasi ya wananchi; na kwa maneno mengine, katika mfumo huu wa kisiasa, wananchi ndio wanaotoa kauli ya mwanzo na ya mwisho katika siku ya upigaji kura kwa kumkabidhi mtu wanayehisi anafaa zaidi kushika hatamu za uendeshaji nchi kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Uchaguzi wa rais wa Iran unadhihirisha kwa maana halisi irada na matakwa ya wananchi, kwa sababu matokeo yoyote yanayotokana na masanduku ya kupigia kura ndiyo yanayoainisha rais mpya wa nchi. Ni kutokana na umuhimu huo ndipo ikashuhudiwa kuanzia saa za awali za upigaji kura, wananchi wa jamii na matabaka tofauti wakijtokeza katika anga ya uchangamfu mkubwa na salama na yenye amani na utulivu kushiriki katika uchaguzi wa 12 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baadhi ya wananchi baada ya kupiga kura

Ni kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kufanyika uchaguzi kwa kuhudhuriwa kwa wingi na wananchi, kwa hamasa, msisimko na uchangamfu na katika mazingira ya amani na usalama ni hazina kwa Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, itakayoipa nchi kinga kubwa na imara.

Kujitokeza kwa wingi wananchi katika uchaguzi na katika anga ya amani na utulivu kunasambaratisha mahesabu ya maadui na kuimarisha zaidi usalama wa taifa na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kieneo na kimataifa duniani.../