Rais Rouhani anaongoza katika matokeo ya awali, akifuatiwa na Raeisi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29310-rais_rouhani_anaongoza_katika_matokeo_ya_awali_akifuatiwa_na_raeisi
Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi uliofanyika jana hapa nchini Iran linaendelea na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa, Rais wa sasa Hassan Rouhani anaongoza akifuatiwa na Sayyid Ibrahim Raeisi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2017 23:30 UTC
  • Rais Rouhani anaongoza katika matokeo ya awali, akifuatiwa na Raeisi

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi uliofanyika jana hapa nchini Iran linaendelea na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa, Rais wa sasa Hassan Rouhani anaongoza akifuatiwa na Sayyid Ibrahim Raeisi.

Akitangaza matokeo hayo ya awali muda mchache uliopita, Abdolreza Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kuwa, baada ya kura milioni 25 kuhesabiwa, Hassan Rouhani anaongoza akiwa na kura milioni 14 akiafuatiwa na Sayyid Ibrahim Raeisi ambaye amejikusanyika kura milioni kumi. 

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran ambayo ndio msimamizi wa uchaguzi wa Iran imetangaza kuwa, zoezi la kuhesabu kura hizo lililoanza jana usiku mara tu baada ya kukamilika zoezi la upigaji kura, linaendelea na kwamba, kuna uwezekano wa zoezi hilo kukamilika leo mchana na matokeo ya mwisho kutangazwa. 

Jana Wairani 56,410,234 waliokuwa wametimiza masharti ya kupiga kura walijitokeza kwenye vituo mbalimbali kutumbukiza kura zao katika masanduku ya kupigia kura za chaguzi zilizofanyika nchini. 

Rais Rouhani (kushoto) na Sayyid Ibrahim Raisi, wagombea wakuu wa uchaguzi wa rais

Kutokana na watu kujitokeza kwa wingi mno katika uchaguzi wa jana, Tume ya Uchaguzi ya Iran ililazimika kuongeza muda wa upigaji kura ambapo baadhi ya wananchi walikuwa vituoni mpaka saa sita za usiku kwa majira ya hapa nchini.

Licha ya kuwa kiti cha Urais kinawaniwa na wagombea wanne lakini mchuano mkali unatarajiwa kushudiwa kati ya Rais wa sasa Hassan Rouhani na Sayyid Ibrahim Raeisi, Msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS. Rais Rouhani anatoka katika mrengo wa wapenda mageuzi huku Sayyid Ibrahim Raeisi akiwania kiti hicho kutoka mrengo wa wahafidhina. Wagombea wengine wa kiti cha Urais ni Mostafa Aqa-Mirsalim mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu na Makamu wa Zamani wa Rais wa Iran, Mostafa Hashemi-Taba.