Rais Hassan Rouhani atangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa jana
Tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imemtangaza Rais Hassan Rouhani kuwa mshindi wa duru ya 12 ya uchaguzi wa rais iliyofanyika Ijumaa ya jana kwa kupata asilimia 57.
Kwa mujibu wa Abdolreza Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Rais Rouhani ameibuka mshindi kwa kupata kura milioni 23 ambazo ni sawa na asilimia 57. Huku Sayyid Ibrahim Raeisi akishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 15 ambayo ni sawa na asilimia 38.5. Tume ya Uchaguzi ya Iran imetangaza kuwa, katika uchaguzi wa duru ya 12 ya rais hapo jana kulipigwa kura milioni 41220131, ambapo Rais Rouhani amepata jumla ya kura milioni 23 laki tano 49 elfu 616, huku Sayyid Ibrahim Raeisi akipata kura milioni 15 laki saba 86 elfu na 449.
Aidha Mostafa Aqa-Mirsalim amepata kura laki nne 78 elfu na 215 huku Mostafa Hashemitaba akipata kura laki mbili 15 elfu na 450. Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Iran, ushiriki wa wapiga kura katika uchaguzi wa jana ulifikia asilimia 71.