Mar 13, 2016 03:31 UTC
  • Ayatullah Rafsanjani: Umoja baina ya Shia na Suni ni jambo lenye ulazima

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema umoja baina ya Shina na Suni una umuhimu mkubwa mno hususan katika hali na mazingira tete na hasasi yanayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni.

Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani, aliyasema hayo jana katika majlisi ya maombolezo ya Bibi Fatimatuz-Zahra (SA) iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa waumini wa matabaka mbalimbali.

Huku akibainisha kwamba vita baina ya Shia na Suni ndio jambo wanalolitamani maadui wa Uislamu, Ayatullah Rafsanjani amesema haifai kuchochea mizozo na mapigano baina ya Shia na Suni kwa kukuza masuala ya hitilafu, bali badala yake inapasa kutumia mantiki na mwenendo wa busara ili uhusiano baina ya Waislamu uzidi kuwa imara siku baada ya siku.

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa kuimarishwa uhusiano baina ya Shia na Suni kuna mahusiano na mfungamano mkubwa na kupata nguvu na uwezo Waislamu duniani; na akasisitiza kwamba: Ikiwa Shia na Suni wataweza kufikia hatua ya kuwa na mshikamano na wakawa kitu kimoja masuala na matatizo yao mengi yatatatuka na wataweza kuwa nguvu kubwa mno na yenye taathira katika uga wa kimataifa.../

Tags