Iran yalaani njama za mashambulio ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Makkah
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30904-iran_yalaani_njama_za_mashambulio_ya_kigaidi_dhidi_ya_msikiti_wa_makkah
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amelaani vikali njama chafu za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Makkah na kuwataka Waislamu kuwa macho na kufanya juhudi kubwa za kupambana na ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2017 09:37 UTC
  • Iran yalaani njama za mashambulio ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Makkah

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amelaani vikali njama chafu za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Makkah na kuwataka Waislamu kuwa macho na kufanya juhudi kubwa za kupambana na ugaidi.

Bahram Qassemi ameyasema hayo Jumamosi ya leo ambapo sambamba na kuashiria njama za kushambulia Haramu tukufu ya Makkah ambazo zinaonekana kufeli amesema kuwa, kwa mara nyingine ugaidi ambao unaonekana kuongezeka na kuilenga dunia nzima hususan katika nchi za Waislamu na eneo la Mashariki ya Kati umedhihirisha kwamba hautambui dini, mipaka wala jiografia, kama ambavyo pia unalenga hata maeneo matakatifu ya Waislamu na Uislamu kwa ujumla.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine amezitaka tawala zote hususan za eneo kuwa makini na njama hizo chafu za kutoa pigo kwa dini hii ya mbinguni. Hii ni katika hali ambayo msemaji wa usalama wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia amenukuliwa akitangaza habari ya kusambaratishwa shambulio la kigaidi ambalo lilikaribia kutekelezwa dhidi ya msikiti wa Makkah kwa kuwalenga wafanyaziara na watu waliokuwa wanaswali msikitini hapo. Kwa mujibu wa habari hiyo, mashambulizi hayo ya kigaidi yalikuwa yamepangwa kutekelezwa katika sehemu tatu za msikiti huo. Jana Ijumaa gaidi mmoja aliyekuwa na nia ya kwenda kujiripua katika msikiti huo ambao ni kibla cha Waislamu alipambana na maafisa usalama waliojaribu kumkamata baada ya kugundua sehemu aliyokuwa amejificha lakini baadaye akaamua kujiripua baada ya kuona amezidiwa nguvu.

Msikiti wa Makkah unaokabiliwa na njama chafu za Uwahabi

Katika tukio hilo, askari wa usalama wa Saudia waliwanasa watu watano akiwemo mwanamke mmoja kwa kuhusika na njama hiyo.