Safavi: Kuna hatari ya kutokea fitna mpya Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31302-safavi_kuna_hatari_ya_kutokea_fitna_mpya_ghuba_ya_uajemi
Mshauri Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya Marekani, Saudi Arabia na Wazayuni kushindwa vibaya katika nchi za Iraq na Syria, hivi sasa kuna uwezekano kundi hilo likaanzisha fitna mpya katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 03, 2017 23:12 UTC
  • Safavi: Kuna hatari ya kutokea fitna mpya Ghuba ya Uajemi

Mshauri Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya Marekani, Saudi Arabia na Wazayuni kushindwa vibaya katika nchi za Iraq na Syria, hivi sasa kuna uwezekano kundi hilo likaanzisha fitna mpya katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Mtandao wa habari wa Sepah News umemnukuu Meja Jenerali Sayyid Yahya Safavi akisema hayo jana Jumatatu na huku akiashiria ushindi mkubwa uliopatikana nchini Iraq baada ya kukombolewa mji wa Mosul amesema: Kwa hakika, kushindwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchni Iraq kuna maana ya kushindwa kundi la Marekani, Saudi Arabia, Uturuki, Jordan, Qatar na Wazayuni katika eneo hili.

Meja Jenerali Safavi ameongeza kuwa, licha ya kushindwa magaidi wa ISIS nchini Iraq, lakini vitendo vya uvunjifu wa amani vinatarajiwa kuendelea nchini humo kwani ni jambo lililo wazi kwamba Wamarekani hawawezi kuiachia hivi hivi Iraq.

Sehemu ya nguvu za kijeshi za Iran

 

Amebainisha kuwa, kushindwa muungano huo unaoongozwa na Marekani katika nchi za Iraq na Syria na kushindwa Saudia nchini Yemen bila ya shaka kutawalazimisha kutafuta njia za kulipiza kisasi.

Amesema, kushindwa siasa zao hizo ndiko kulikoifanya Saudi Arabia ifikirie kuanzisha NATO ya nchi za Kiarabu kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, Uingereza na Wazayuni; "NATO ya Kiarabu" ambayo imefeli hata kabla ya kuanzishwa kwake.

Mshauri Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, eneo la magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ni muhimu sana na ni la kiistratijia kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba kupanuliwa njia za reli, kuwa na ushawishi wa kisiasa na kusafirisha gesi na mafuta ya Iran kupitia Iraq, Syria hadi bahari ya Mediterranean sambamba na kuongeza kiwango cha usafirishaji bidhaa za Iran nchini Iraq hadi kufikia dola bilioni 20 ni miongoni mwa fursa nzuri kwa Iran katika siku za usoni.