Rohani: Taifa la Iran litayashinda madola ya kibeberu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa taifa la Iran limeonesha kuopitia uwezo wake, umoja na udiplomsia wake kuwa litashinda njama za madola makubwa ya kibeberu duniani.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo akihutubia Tamasha la Afya mjini Tehran na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran si tu kwamba, wamesimama kidete mbele ya matatizo yote, bali pia wanayasaidia mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kama ya Iraq na Syria. Ameongeza kuwa, Iran imekuwa ikiyasaidia mataifa ya Syia na Iraq hata katika vipindi vya hali ngumu kabisa ya kiuchumi.
Rais Rouhani amesema kuwa, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi hasimu za Mashariki ya Kati zinaifanyia uadui Jamhuri ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, Iran inawahitajia wananchi, uongozi wake wa juu na kujitolea kwa maafisa wake kwa ajili ya kuendelea kuwashinda maadui.
Vilevile amezungumzia maendeleo ya sekta ya afya nchini Iran na kusema kuwa: Hii leo magonjwa sugu na hatari yanatibiwa katika Jamhuri ya Kiislamu na wagonjwa wengi sasa hawaendi katika nchi za Magharibi kwa ajili ya matibabu. Amesisitiza kuwa, Iran sasa imekuwa marejeo ya kutibu magonjwa mbalimbali, na kwamba wagonjwa wengi kutoka nchi mbalimbali wanakuja hapa nchini kwa ajili ya kupata matibabu.