Rouhani: Uwezo wa Iran umetokana na kupiga hatua katika uga wa sayansi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua ya Iran ya kufanya majaribio ya roketi la kupeleka satalaiti katika anga za mbali kwa mafanikio na kubainisha kuwa, mafanikio kama haya ya kisayansi ndiyo yameipa Iran uwezo na izza mkabala wa adui.
Rais Rouhani amesema sayansi za anga za mbali na teknolojia ni masuala yenye umuhimu mkubwa kwa taifa hili na kusisitiza kuwa, kadri Iran ya Kiislamu inavyozidi kupiga hatua katika uga wa sayansi, ndivyo inavyozidi kupata nguvu, heshima na izza.
Hapo jana Iran ilifanya majaribio yaliyofanikiwa ya roketi la Simorgh linalotumiwa kupeleka satalaiti angani.
Roketi la Simorgh lina uwezo wa kupeleka angani satalaiti yenye uzito wa kilo 250 umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini.
Katika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais wa Iran amesema: "Katika kipindi hiki cha utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama JCPOA, Tehran itatumia kila fursa iliyopo kupiga hatua kubwa zaidi katika uga wa sayansi, kwa kutegemea wataalamu waliobobea wa hapa nchini."
Majaribio hayo yalifanyika sambamba na uzinduzi wa Kituo cha Taifa cha Masuala ya Anga cha Imam Khomeini katika mlolongo wa sherehe za kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Ali bin Musa al Ridha (AS).
Itakumbukwa kuwa, Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa ijulikanayo kwa jina la Omid (Tumaini) mwaka 2009.