Watu 13 wafariki dunia katika maafa ya mafuriko kaskazini mwa Iran
Watu wasiopungua 13 wamefariki dunia hapa nchini Iran na makumi ya wengine kujeruhiwa huku mali za watu zikiharibiwa kufuatia maafa ya mafuriko yaliyoyakumba maeneo ya kaskazini mwa nchi.
Mkuu wa Shirika la Kupambana na Majanga ya Kimaumbile amethibitisha kuaga dunia watu kumi na tatu kufuatia baa hilo la mafuriko na kusema kwamba, maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo makubwa ni mikoa ya Golestan, Khorasan Razavi na Khorasan Kaskazini.
Ismail Najjar, Mkuu wa Shirika la Kupambana na Majanga ya Kimaumbile amesema kuwa, watu wanane wamepoteza maisha katika mkoa wa Khorasan Razavi uliko kaskazini mashariki mwa nchi, wanne katika mkoa wa Golestan na kwamba, mtu mmoja amepoteza maisha katika mkoa wa Khorasan Kaskazini.
Amesema kuwa, mafuriko hayo ya jana yaliyoikumba mikoa hiyo yalikuwa makubwa mno na kwamba, yamesababisha pia hasara kubwa ya mali za watu ikiwa ni pamoja na kusomba magari na kuharibu mashamba ya mpunga.
Ismail Najjar amesema kuwa, bado kuna watu kadhaa ambao hadi sasa hawajulikani walipo baada ya mafuriko hayo na kwamba, timu za uokozi zinaendelea na kazi ya kuwatafuta.
Wakati huo huo, mafuriko yaliyotokea pia katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran yamesababisha hasara kubwa baada ya kuharibu miundo mbinu ya mkoa huo. Ikumbukwe kuwa, siku ya Alkhamisi na jana Ijumaa, mvua kubwa ilinyesha katika mikoa ya Golestan, Gilan, Khorasan Razavi, Khorasan Kaskazini na Semnan na kusababisha mafuriko makubwa.