Rais Rouhani: Iran iko tayari kushirikiana kisayansi na nchi za Kiislamu
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitizia ulazima wa umoja na ushirikiano wa nchi za Waislamu ili kuondoa machafuko duniani na kupatikane amani ya kudumu.
Rais Rouhani ameyasema hayo kwenye hotuba yake aliyoitoa leo katika mkutano wa kwanza wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kuhusu sayansi na teknolojia katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana.
Rais Rouhani amesema, udhaifu, kubaki nyuma na kukosekana umoja wa nchi za Waislamu ni mambo ambayo yanapelekea iwe vigumu kufikia amani na ustawi jumuishi. Rais wa Iran amesema, ushirikiano wa nchi za Ulimwengu wa Kiislamu ni jambo linaloweza kupelekea kuangamizwa ujinga, umasikiini na vita duniani.
Rais Rouhani amesema ushirikiano katika uga wa sayansi na teknolojia una umuhimu wa kisiasa na kijamii. Aidha amesema nchi za Kiislamu leo zinahitaji umoja kwani zinakabiliana na migogoro kadhaa kama vile jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, ukatili wa Mabuddha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya pamoja na maafa ya kibinadamu yaliyosababishwa na makundi yenye misimamo mikali huko Syria na Iraq na vile vile kuendelea hujuma za Saudia nchini Yemen.
Rais wa Iran amesema, kikao cha leo cha OIC kinaweza kuwa msingi wa kihistoria wa ushirikiano wa kisayansi katika ulimwengu wa Kiislamu. Aidha amebainisha kuwa Iran iko tayari kushirkiana na nchi zote za Kiislamu katika uga wa sayansi, teknolojia na ubunifu.