Ayatullah Shahroudi: Uwezo wa kiulinzi wa Iran hauwezi kudhoofishwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35657-ayatullah_shahroudi_uwezo_wa_kiulinzi_wa_iran_hauwezi_kudhoofishwa
Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, mashinikizo ya Marekani ya kutaka kuuwekea mipaka uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Iran hayakubaliki na kusisitiza kwamba uwezo wa kiulinzi wa Iran hauwezi kudhoofishwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2017 11:59 UTC
  • Ayatullah Shahroudi: Uwezo wa kiulinzi wa Iran hauwezi kudhoofishwa

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, mashinikizo ya Marekani ya kutaka kuuwekea mipaka uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Iran hayakubaliki na kusisitiza kwamba uwezo wa kiulinzi wa Iran hauwezi kudhoofishwa.

Ayatullah Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi ameashiria matamshi yasiyo ya kidiplomasia yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran na kueleza kwamba katika porojo lake, Trump hakuzungumzia jambo jengine zaidi ya tuhuma hewa.

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran aidha amesema hasira za Trump dhidi ya Iran zinatokana na kushindwa siasa za Marekani katika Mashariki ya Kati na akabainisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikikwamisha kutekelezwa sera za kibabe za Marekani katika eneo.

Ayatullah Shahroudi amebainisha pia kwamba Marekani imekasirika kutokana na kushindwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh katika eneo na kuongeza kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ni miongoni mwa nguvu kuu zilizochangia kushindwa Daesh katika Mashariki ya Kati.

Askari wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)

Rais wa Marekani Donald Trump, jana alitoa matamshi machafu na kurudia tuhuma hewa za huko nyuma dhidi ya Iran, ambapo mbali na kutothibitisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA amedai kwa mara nyengine tena kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwenye orodha ya taasisi zitakazowekewa vikwazo vipya na serikali ya Washington.

Ikumbukwe kuwa, kwa ombi rasmi la serikali za Iraq na Syria, Jeshi la Sepah limekuwa likitoa ushauri wa kijeshi katika kupambana na makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi hizo; hatua ambayo haijamfurahisha hata kidogo Rais wa Marekani.../