Rais Rouhani: Wamarekani wanataka kuwavunja moyo wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36060-rais_rouhani_wamarekani_wanataka_kuwavunja_moyo_wananchi_wa_iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wanataka kuwavunja moyo wananchi wa Iran kuhusu masuala yao ya kiuchumi na hiyo ndiyo njama yao kuu ya kuzuia maendeleo ya taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2017 01:14 UTC
  • Rais Rouhani: Wamarekani wanataka kuwavunja moyo wananchi wa Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wanataka kuwavunja moyo wananchi wa Iran kuhusu masuala yao ya kiuchumi na hiyo ndiyo njama yao kuu ya kuzuia maendeleo ya taifa hili.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo usiku wa kuamkia leo hapa mjini Tehran na huku akiwashukuru wananchi wa Iran kwa kulinda mshikamano wao wa kitaifa, amelaani njama za mabeberu za kuzusha machafuko na vitendo vya kigaidi katika eneo hili na kuongeza kuwa, licha ya kuweko njama zote hizo za maadui, lakini eneo hili hivi sasa limeanza kutoka katika hali ngumu iliyozushwa na mabeberu hao.

Rais Rouhani ameashiria pia njama za mabeberu wa dunia za kujaribu kuvuruga mipaka ya kijiografia ya nchi za eneo hili na kuongeza kuwa, njama za mabeberu hao zimeshindwa pia katika upande huo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, wakati mabeberu wa dunia wanaendelea na njama zao za kuzusha mizozo na mifarakano katika eneo hili ili kuimarisha soko lao la silaha, wajibu wetu sisi ni kutafuta njia za kukabiliana na njama hizo kupitia kuondoa hitilafu na kuzidisha ushirikiano baina ya nchi za eneo hili.