Velayati: Lengo la Iran na Syria ni kulinda mhimili wa muqawama
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Katika Masuala ya Kimataifa amesema kuwa lengo la Iran na Syria ni kulinda mhimili wa muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati na kusimama kidete kukabiliana na Uzayuni na waungaji wake mkono.
Ali Akbar Velayati amesema kuwa Iran na Syria zina stratejia kuu za pamoja kuhusu muqawama na kuongeza kuwa ushirikiano wa pande zote kati ya Iran na Syria umewafanya viongozi wa Marekani na Wazayuni watambue kuwa kile ambacho wamekuwa wakitaka kuitwisha serikali na wananchi wa Syria si kingine ghairi ya njozi tu. Velayati aliyasema hayo jana baada ya mazungumzo na Walid al Muallim Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria huko Damascus.
Mshauri wa Ayatullah Khamenei katika masuala ya kimataifa ameashiria ushindi wa jeshi na wananchi wa Syria huko Deir -Zor na katika maeneo mengine ya Syria na kueleza kuwa: Iran na Syria siku zote zimekuwa zikishirikiana na kufanya uratibu kwa pamoja.
Walid al Muallim Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria kwa upande wake alisisitiza kuwa uhusiano imara na wa kistratejia kati ya Syria na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si siri na kwamba uhusiano huo unajumuisha nyanja zote. Walid al Muallim amesema kuwa Syria inajifakharisha kuona kuwa Iran ipo katika mhimili wa muqawama na kwamba Iran na mshirika wa ushindi wa wananchi na jeshi la Syria. Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Katika Masuala ya Kimataifa Jumapili usiku aliwasili Syria akitokea Lebanon ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo baada ya kumaliza ziara yake huko Lebanon.