Rouhani: Uhasama wa Saudia ni mbinu ya kuficha changamoto zinazoikabili
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Saudi Arabia kushadidisha uhasama na uadui wake dhidi ya Tehran ni mbinu ya kujaribu kuficha kufeli kwake katika masuala ya kieneo sawa na changamoto zinazoukabili utawala wa Riyadh ndani ya nchi hiyo.
Rais Rouhani amesema Riyadh inajaribu kuyapatia ufumbuzi matatizo mawili makuu yanayoikabili kwa sasa. Amesema changamoto ya kwanza inayowakabili watawala wa Riyadh ni kufeli kwa sera zao za kieneo, katika nchi za Qatar, Iraq, Syria na hivi karibuni Lebanon.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa, tatizo la pili linaloukabili utawala wa Aal-Saud ni changamoto za ndani ya nchi hususan mikwaruzano miongoni mwa wanawafalme.
Rais wa Iran amesema changamoto hizi ndizo zimeifanya Riyadh ishadidishe uhasama wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akisisitiza kuwa, sera ya nje ya Iran imejengeka katika misingi ya kutafutia ufumbuzi changamoto za kieneo kupitia mazungumzo na wala sio vitisho; akisema mfano hai ni namna uhusiano wa kieneo kati ya Tehran na Uturuki, Iraq, Afghanistan, Pakistan na Qatar unavyozidi kuimarika.
Kauli ya Rouhani ni radiamali kwa matamshi ya kijuba yaliyotolewa hivi karibuni na Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia katika mahojiano na gazeti la New York Times yaliyochapishwa Alkhamisi iliyopita.
Katika mahojiano hayo, Bin Salman alifananisha kuimarika ushawishi wa Iran katika eneo na sera za Ujerumani katika enzi za Hitler, huku akitishia kuleta vita 'mlangoni pa Iran'.