Zarif: Magaidi wazawa wa Magharibi ndio wanaowaua watoto Syria, Iraq
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka nchi za Magharibi zitoe ufafanuzi kuhusu ni kwa nini wimbi la watoto wanaozaliwa, kulelewa na kupata elimu katika nchi hizo ndio wanaoongoza katika mauaji yanayofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) dhidi ya watoto wa Syria na Iraq.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo Jumapili katika kongamano la kutathmini mafanikio ya barua mbili zilizotumwa na Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kwa vijana wa Magharibi katika miezi ya Januari na Novemba mwaka 2015.
Amehoji: "Kwa nini waliozaliwa na kupata elimu katika nchi za Magharibi ndio wanaoongoza katika kuwachinja watoto wa Syria na Iraq? Kwa nini watu hawa wanaonyesha ukatili na ukosefu wa utu kiasi hiki? Nchi za Magharibi zitatoa ufafanuzi gani kuhusiana na malezi ya aina hii?"
Kadhalika Dakta Zarif amebanisha kuwa, Wamagharibi walianza kampeni za kueneza chuki dhidi ya Uislamu, Ushia na Iran katika miaka ya 90, hata kabla ya kuzaliwa kundi la ukufurishaji la Daesh.

Wakati huo huo, Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa akihutubia mkutano huo amesema kuwa nchi za Magharibi zinafanya juu chini kupanda mbegu za chuki na migawanyiko miongoni mwa Waislamu kwa shabaha ya kufufua ujahili wa zama za kabla ya ujio wa Uislamu.
Katika barua zake kwa vijana wa Magharibi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwataka vijana hao kuusoma Uislamu halisi, huku akifafanua sababu za vijana wa Magharibi kuwa wepesi kujiunga kwa wingi na magenge ya kitakfiri hususan Daesh katika nchi za Syria na Iraq.