Iran katu haitaruhusu vituo vyake vya kijeshi vikaguliwe
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amesisitiza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitaruhusu vituo vyake vya kijeshi vikaguliwe na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA."
Behrouz Kamalvandi amongeza kuwa suala la kukaguliwa vituo vya nyuklia vya Iran haliko katika kadhia ya protokali ziada au katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Aidha amepuuzilia mbali masharti manne yaliyotolewa na Rais wa Marekani kuhusu kuendelea kufungamana nchi yake na JCPOA na kuongeza kuwa: "Miaka ya nyuma, baada ya kukaguliwa vituo vya kijeshi kama kile cha Parchin, faili hilo lilifungwa na sasa hakuna suala lolote lilolowasilishwa na IAEA ili kulazimisha kukaguliwa vituo vya kijeshi vya Iran."
Siku ya Ijumaa, Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine alirefusha muda wa kusitisha vikwazo vya nyuklia vya Iran licha ya kutoridhishwa na makubaliano hayo. Trump amesema iwapo mazungumzo mapya hayatafanyika kuhusu mapatano ya JCPOA basi hatayaidhinisha baada ya miezi mitatu ijayo. Mtawala huyo wa Marekani anataka kadhia ya makobora ya kujihami ya Iran iingizwe katika mapatano hayo ya nyuklia jambo ambalo Iran imelipinga vikali.
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amesema Tehran itaendelea kushirikian na IAEA kwa mujibu wa mapatano yaliyopo ya kimataifa na si vinginevyo.