Kamalvandi: Shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa mujibu wa sheria
(last modified Fri, 26 Nov 2021 08:04:36 GMT )
Nov 26, 2021 08:04 UTC
  • Kamalvandi: Shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa mujibu wa sheria

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema, shughuli zote za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu zinafanyika kulingana na sheria, lakini kuna baadhi wanaotafuta kila njia ili waituhumu Iran.

Behrouz Kamalvandi, msemaji na mkuu wa masuala ya kimataifa, ya kisheria na bunge wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amezungumzia safari ya karibuni ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA hapa mjini Tehran na akasema, madola yenye nguvu duniani yameupa sura ya kisiasa upande mmoja wa shughuli za nyuklia za Iran zinazofanyika kwa malengo ya amani, lakini inafahamika kuwa Iran inataka kufaidika na teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani na imetekeleza majukumu yake yote kulingana na taratibu za ukaguzi na usimamizi za IAEA.

Kamalvandi amekumbusha kuwa, mashirika ya kimataifa yako chini ya satua na ushawishi wa madola makubwa; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshatanabahisha mara kadhaa kuhusu mwenendo usio wa sawa wa wakala wa atomiki na kuvitaka vyombo vya habari viwe macho kwa ajili ya kuzima njama za Marekani na waitifaki wake dhidi ya Iran.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami (kushoto) na Mkuu wa IAEA Rafael Grossi

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebainisha kuwa, Iran imekuwa na matakwa yake kadhaa ambayo imeyaeleza katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA; na hatua nzuri zimepigwa katika mazungumzo hayo, hata hivyo haikuwezekana kufikia hitimisho juu ya masuala yote kutokana na uhaba wa muda.

Siku ya Jumanne, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki alifanya safari hapa mjini Tehran, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran kuhusu kuendelezwa mashirikiano kati ya Tehran na IAEA katika uga wa shughuli za nyuklia za Iran.../

Tags