Iran yalaani vikali mpango wa Marekani kutuma wanajeshi Syria
Rais Hassan Rouhani wa Iran amelaani vikali hatua ya Marekani kutuma askari wake nchini Syria na kusmea: "Mpango wa Marekani ni kinyume cha sheria za kimataifa na ni njama dhidi ya usalama na mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya Syria na eneo."
Baada ya kushindwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Syria na Iraq, Marekani imetangaza kuwa, inashirikiana na kaumu ya Wakurdi Wasyria kuunda jeshi jipya ndani ya Syria.
Rais Hassan Rouhani akizungumza Jumanne na Hammouda Youssef Sabbagh Spika wa Bunge la Syria aliye safarani mjini Tehran, amesema kuendeleza vita dhidi ya magaidi na kukabiliana na uingiliaji wa madola ya kigeni ni maudhui muhimu kwa taifa la Syria. Aidha amesema kunapaswa kuwepo jitihada za kuhakikisha wakimbizi Wasyria wanarejea katika nchi yao ili kushiriki katika kuijenga upya.
Aidha amesema Iran daima itaendelea kuwaunga mkono watu wa Syria ili nchi hiyo iendelee huku akisisitiza kuendelea mchakatao wa mazungumzo ya kutafuta amani Syria.
Kwa upande wake Hammouda Youssef Sabbagh Spika wa Bunge la Syria ameishukuru Iran kwa kuendelea kuunga mkono nchi yake katika vita dhidi ya ugaidi na katika ujenzi mpya wa nchi hiyo.
Aidha ameashiria njama mpya za Marekani dhidi ya Syria hasa kutumwa vikosi vya Marekani katika ardhi ya Syria na kusema serikali ya nchi yake imetoa ombi rasmi la kutaka wanajeshi wa Marekani nchini humo wanondoke.
Spika wa Bunge la Syria amefika Iran kuhudhria mkutano wa Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu.