Magari ya Mercedes Benz E-Class sasa kuundwa nchini Iran
Shirika la Mercedes-Benz la Ujerumani litaanza tena kutengeneza magari yake nchini Iran kuanzia mwaka mpya wa Kiirani utakaoanza Machi 21.
Kwa mujibu wa taarifa Mercedes-Benz, ambayo ni sehemu ya Shirika la Daimler AG, imepanga kutengeneza magari 2,500 aina ya E-class katika kipindi cha mwaka moja ambapo asilimia 20 ya uundwaji utafanyika hapa Iran na iliyosalia kuingizwa nchini kama vipuri katika muundo wa CKD.
Shirika la Mercedes-Benz lina historia ndefu nchini Iran ambapo lilianza biashara yake humu nchini muongo wa 1950 wakati lilikuwa likiuza magari hadi 10,000 kwa mwaka. Shirika hilo lilisitisha shughuli zake nchini Iran mwaka 2012 wakati nchi za Ulaya zilifuata Marekani katika kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo.
Taarifa zinasema hivi sasa kiwanda cha kuunda magari ya Mercedes-Benz nchini Iran kinaandaliwa upya kwa ajili ya kuunda magari mapya.
Januari mwaka 2016 Shirika la Daimler AG lilfikia mapatano na washirika wake nchini Iran ambao ni Shirika la Iran Khodro Diesel na Shirika la Mammut kwa lengo la kuanza uundwaji wa magari yake nchini.
Iran ambayo yenyewe pia ina viwanda kadhaa vya magari yanayoundwa hapa nchini ni soko kubwa kwa mashirika ya kimataifa ya utengenezaji magari. Shirika lingine la Ujerumani la Volkswagen nalo lilianza kuuza tena magari yake nchini Iran mwaka jana huku mashirika ya PSA na Renault ya Ufaransa nayo yakiwa mbioni kujiimarisha tena nchini baada ya kupoteza soko wakati wa vikwazo. Siku ya Jumanne Shirika la Peugeot lilitangaza kuwa mwaka jana liliuza magari 444,600 nchini Iran huku Shirika la Renault likitangaza ongezeko la asilimi 54 ya uuzaji magari yake nchini mwaka jana.