Tamasha la Kimataifa la Filamu la Fajr la Iran kufanyika Aprili
Tamasha la Kimataifa la Filamu la Fajr la Iran (FIFF) limepangwa kufanyika chini ya miezi miwili ijayo huku idadi kubwa ya filamu ikiwania kushiriki katika tamasha hilo.
Hadi sasa mamia ya watengeneza filamu kutoka ameneo yote duniani wameshawasilisha kazi zao kushiriki katika tamasha hilo la 36 ambalo limepangwa kuanza katika mji mkuu wa Iran, Tehran kuanzia Aprili 19 hadi 27.
Tamasha hilo limeandaliwa na Taasisi ya Sinema ya Farabi ambayo ni kitengo cha Wizara ya Utamaduni na Muongoze wa Kiislamu Iran.
Wakuu wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Fajr la Iran wanasema lengo lao ni kutambua kazi zenye thamani na ubunifu za sinema na kuandaa mazingira ya watengeneza filamu wa kimataifa kubadilishana mawazo.
Aidha wanasema lengo jingine la tamasha hilo ni kusisitiza kuhusu kusambazwa ujumbe wa uadilifu, amani duniani sambamba na kuhimiza maadili mema na thamani za kibinadamu.
Tamasha la Kitaifa la Filamu la Fajr lilifanyika baina ya Februari 1 hadi 10 ambapo filamu bora zilitunukiwa zawadi.