Mar 08, 2018 08:20 UTC
  • Rouhani: Tehran na Ankara zina majukumu mazito ya kuwaokoa watu wa Syria

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Tehran na Ankara zina majukumu mazito ya kuwaokoa raia wa Syria hususan katika eneo la Ghouta Mashariki na kusisitiza kuwa, Kuna udharura wa kufanyika jitihada za kuzuia maafa ya kibinadamu katika eneo hilo.

Dakta Hassan Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan na kuongeza kuwa, Iran na Uturuki ambazo ni nchi mbili za Waislamu na jirani na Syria zinapaswa kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kusitisha vita huko Syria na kurejesha amani nchini humo. 

Amesisitiza kuwa, kuzuia mashambulizi ya maroketi yanayofanywa na magaidi katika eneo la Ghouta Mashariki dhidi ya mji mkuu wa Syria, Damascus na kudhamini usalama kwa mji huo, sambamba na kutayarisha njia salama ya kuondoka raia waliokwama katika eneo hilo na kulisafisha kabisa na magaidi ni baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kurejesha amani na usalama. Rais Rouhani ameitaka serikali ya Uturuki kutumia ushawishi wake kwa ajili ya kutimizwa malengo hayo.

Ghouta Mashariki, Syria

Vilevile ameashiria umuhimu wa ushirikiano wa Iran, Russia na Uturuki huko Syria na kusema: Iran iko tayari kikamilifu kuchukua hatua yoyote inayohitajika kwa ajili ya kusitisha mapigano eneo la Ghouta Mashariki na kutoa misaada ya kibinadamu kwa raia wa eneo hilo kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa 

Vilevile ameitaka serikali ya Uturuki kufanya jitihada za kukomesha mzingiro wa magaidi dhidi ya wanawake na watoto wa miji ya Foua na Kefraya huko kaskazini magharibi mwa Syria. 

Kwa upande wake, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ameitaja hali ya eneo la Ghouta Mashariki kuwa ni maafa makubwa na kusema: Iran na Uturuki ambazo ni nchi mbili kubwa za Waislamu zinalazimika kufanya juhudi za kukomesha maafa hayo.  

Tags