Ndege ya Uturuki yaanguka nchini Iran
-
Picha za awali za ndege ya Uturuki iliyopata ajali nchini Iran (Picha kwa hisani ya Fars News)
Ndege moja binafsi ya Uturuki iliyokuwa inasafiri kutoka Sharjah, Imarati kuelekea Istanbul Uturuki imeanguka karibu na Shahr-e Kord katika mkoa wa Chaharmahal va Bakhtiari kusini magharibi mwa Iran.
Taarifa zinasema kuwa, ndege hiyo binafsi ilikuwa na watu 11 na kuna hofu kuwa watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo wamepoteza maisha.
Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Taasisi ya Ndege ya Iran amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa ndege hiyo imeanguka karibu na Shahr-e Kord.
Naye Shahin Fat-hi, naibu wa mkuu wa operesheni wa taasisi ya uokoaji na misaada ya Iran amesema, timu saba zimetumwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuchunguza hali halisi ilivyo na iwapo kuna mtu yeyote aliyepona au la.
Kwa upande wake shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, leo jioni ndege moja binafsi aina ya Bombardier mali ya Uturuki ambayo ilikuwa inatokea Sharjah Imarati, kuelekea Istanbul Uturuki imepotea katika rada na kuanguka wakati ilipokuwa inapita katika anga ya Iran.
Hata hivyo, shirika la habari la Tasnim limemnukuu Reza Jaafarzadeh, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Taasisi ya Ndege ya Iran akisema kuwa idadi rasmi ya watu waliokuwemo kwenye ndege hiyo ilikuwa bado haijaripotiwa kwao. Taarifa za awali zinaonesha kuwa ndege hiyo ilikuwa na watu 11.