Kamanda wa SEPAH: Israel haiwezi kuthubutu kuichokoza Iran
Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna uthubutu wa kuzusha chokochoko dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu wala uwezo wa kuhimili matokeo mabaya ya uchokozi huo.
Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, kamanda wa makao makuu ya Kikosi cha Khatam al-Anbiya, aliyasema hayo jana Jumapili katika mazungumzo na maafisa usalama na wataalamu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, SEPAH (IRGC).
Kamanda huyo wa SEPAH ameashiria mafanikio ya Iran ya kusambaratisha kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo hili, sambamba na mchango wake katika kurejesha amani na utulivu nchini Syria na Iraq na kubainisha kuwa, Tehran imeimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kujihami, kwa lengo la kuzima chokochoko za kijeshi na kiusalama dhidi yake.
Meja Jenerali Gholam Ali Rashid ameionya Marekani dhidi ya kujiingiza katika kinamasi kitakachosababishwa na sera zake za kuchochea na kuzusha migogoro na kuisukuma Israel katika vita vya kijeshi.
Kamanda huyo wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Marekani na utawala haramu wa Israel zimefanya juu chini kuhakikisha kuwa kadhia yenye umuhimu mkubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu yaani kadhia ya Palestina inasahaulika, kwa kuunda muungano wa Waarabu-Israel-Wamagharibi.