Rais Rouhani: Umoja wa taifa la Iran umewashangaza maadui
(last modified Wed, 21 Mar 2018 04:33:59 GMT )
Mar 21, 2018 04:33 UTC
  • Rais Rouhani: Umoja wa taifa la Iran umewashangaza maadui

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ujumbe wa mwaka mpya wa 1397 Hijria Shamsia akisema kuwa, mwaka uliomalizika wa 1396 ulikuwa mwaka wa mafanikio na ushindi wa taifa kubwa la Iran katika nyanja mbalimbali licha ya njama zote za wanaoitakia mabaya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema kuwa umoja na mshikamano wa taifa la Iran umewastaajabisha maadui wote na kuwalazimisha wakiri adhama na utukufu wa taifa hilo. 

Rais Rouhani ambaye alikuwa katika safari ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na mtetemeko wa ardhi ya Kermanshah huko magharibi mwa Iran, amesema kuwa taifa la Iran daima limekuwa likitengenza amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani, na katika mwaka uliomalizika liliweza kuimarisha amani na utulivu Mashariki ya Kati kwa kushirikiana na mataifa ya Iraq, Syria na Lebanon kutokana na jitihada zake kubwa, askari wenye ikhlasi na udiplomasia makini. 

Sikukuu ya Nowruz

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaambia Wairani kwamba: Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwaka mpya wa 1397 Hijria Shamsia utakuwa mwaka wa uzalishaji wa kitaifa, kuunga mkono bidhaa za Kiirani na mwaka wa kutengeneza ajira na ustawi. 

Vilevile amelipa mkono wa kheri ya mwaka mpya taifa la Irani, Wairani wanaoishi nje ya nchi na kaumu na nchi zote jirani zinazosherehekea sikukuu ya Nowruz. 

Mwaka mpya wa 1397 Hijria Shamsia umeanza leo nchini Iran ambapo Wairani kote duniani wanasherehekea sikukuu hiyo ya Nowruz.