Ayatullah Kermani: Iran imesimama kidete dhidi ya mfumo wa ubeberu na uistikbari
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama kidete dhidi ya mfumo wa ubeberu na uistikbari kwa kufuata nyayo za Imam Ali AS.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi Kermani ameashiria kukaribia maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Ali AS na kubainisha utukufu na uadilifu wa Mtukufu huyo na akaongezea kwa kusema, "Kwa kufuata njia ya Imam Ali AS, taifa la Iran limeweza kufikia njia ya uokovu, kwa kusimama imara kukabiliana na mfumo wa uistikbari na ubeberu wa ndani."
Kwengineko katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran, Ayatullah Kermani amewataka maafisa wa Iran kununua bidhaa zilizozalishwa hapa nchini, akisisitiza kuwa kuungwa mkono bidhaa za ndani kutainua uchumi wa taifa.
Huku akiashiria hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Kiirani, Ayatullah Mohammad Ali Movahedi Kermani amezitaka kampuni zinazozalisha bidhaa hapa nchini kuboresha bidhaa hizo ili kutoa ushindani kwa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

Katika ujumbe aliotoa kwa taifa kwa mnasaba wa kuingia mwaka mpya wa 1397 hijria shamsia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, aliutangaza mwaka mpya wa 1397 hijria shamsia kuwa mwaka wa "kuunga mkono bidhaa za Iran".
Kadhalika Ayatullah Khamenei alitoa mkono wa heri na baraka kwa wananchi wote wa Iran, hususan familia azizi za mashahidi, majeruhi wa vita pamoja na chipukizi na vijana ambao ni tumaini la kusukuma mbele gurudumu la elimu nchini na kuwatakia wote sikukuu nzuri na ya furaha ya Nouruzi na mwaka mpya wenye wingi wa heri na baraka.