Iran yajiimarisha kijeshi, yaahidi kutoa jibu kali kwa maadui
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema nchi hii inaendelea kuimarisha uwezo wake wa kujihami na kwamba iko tayari kutoa jibu kali kwa maadui iwapo watachukua hatua zozote za uhasama.
Akizungumza Jumanne katika mji wa Tabriz kusini magharibi mwa Iran, Hatami aliwashauri maadui wa Iran wasijaribu uwezo wa kijeshi wa nchi hii kwani watapata jibu kali.
Amesisitiza kuwa, majeshi ya Iran yako tayari kabisa kukabiliana na chokochoko zozote za maadui. Hatami amesema Iran ni nchi yenye uwezo mkubwa wa kujihami katika eneo na kuongeza kuwa, hivi sasa Iran inaweza kufuatilia malengo yake na wakati huo huo kulinda maslahi yake kwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi.
Waziri wa Ulinzi wa Iran aidha amesema maadui ndio waliounda kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na makundi mengine ya magaidi wakufurishaji katika eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati ili kuibua matatizo katika maeneo ya mipaka. Amesema Iran imefanikiwa kuzima njama zote za maadui kupitia uwezo wake mkubwa wa kujihami.
Siku ya Jumamosi, Kamanda wa kituo kikuu cha kijeshi cha Khatam al Anbiyaa (SAW) cha nchini Iran alisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imejiandaa kikamilifu kujihami na kukabiliana na hujuma yoyote dhidi yake na kwamba siasa za Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni za kuzuia mashambulizi.
Meja Jenerali Gholamali Rashid alisisitiza hayo wakati alipokagua vikosi vya majini vya jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC katika fukwe za Makran na visiwa vya Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa, Iran inafuatilia kwa karibu harakati zote zinazotokea katika mipaka yake ya majini na imejiandaa vilivyo kujihami na kukabiliana na hujuma ya aina yoyote ile.