Zarif: Marekani itajuta kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Tehran ina hatua kadhaa ambazo inaweza kuchukua ambazo zitaifanya Marekani ijute kujiondoa katika mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Akizungumza punde baada ya kuwasili mjini New York kuhudhuria kikao kuhusu amani endelevu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Zarif amesema serikali ya Marekani, hasa utawala wa sasa wa Rais Donald Trump, umeshindwa kutekeleza wajibu wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Amesema ni jukumu la nchi za Umoja wa Ulaya zilizoafiki mapatano hayo kuyalinda na kuilazimisha Marekani itekeleze majukumu yake.
Mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yalifikiwa Julai 14 mwaka 2015 baina ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Marekani pamoja na Ujerumani. Mapatano hayo yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016 ambapo Iran ilipunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo ilivyokuwa imewekewa kutokana na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.

Pamoja na serikali ya Marekani kuidhinisha mapatano ya nyuklia wakati wa utawala wa Obama, rais wa sasa wa nchi hiyo ametishia kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo iwapo hayataangaliwa upya, takwa ambalo limepingwa vikali na Iran pamoja na Umoja wa Ulaya.