Iran: Kama Marekani itajitoa katika JCPOA, Tehran itajitoa katika NPT
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43672-iran_kama_marekani_itajitoa_katika_jcpoa_tehran_itajitoa_katika_npt
Katibu wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, iwapo Marekani itajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi Tehran itajitoa katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki, NPT.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2018 09:41 UTC
  • Iran: Kama Marekani itajitoa katika JCPOA, Tehran itajitoa katika NPT

Katibu wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, iwapo Marekani itajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi Tehran itajitoa katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki, NPT.

Mohsen Rezai amesema hayo mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, nchi za Ulaya hazipaswi kuyatia hatarini manufaa yao ya muda mrefu kwa chokochoko za rais wa Marekani, Donald Trump. Ameongeza kuwa, nchi za Ulaya haziwezi kufikia mwafaka na Wamarekani kuhusu kutotekeleza mapatano ya JCPOA.

Ameongeza kuwa, Iran haikubaliani na mipango ya watu wa Ulaya ya kumkinaisha Trump abakie katika mapatano ya JCPOA na kusisitiza kuwa, Marekani imeamua kufuata mkondo mbaya kuhusiana na mapatano hayo ya nyuklia.

Bendera ya pande zilizofanikisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Marekani imo ingawa Trump hivi sasa anatia ulimi puani kuyapinga kana kwamba haikuhusika kabisa kufikiwa kwake

 

Vile vile amesema, Trump ameirudisha nyuma Marekani katika miamala na uhusiano wa kimataifa na kuongeza kuwa, siasa mbovu za Trump zimeirudisha Marekani katika zama za kabla ya vita vikuu vya dunia na kuipotezea uungaji mkono wa kimataifa.

Mapatano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, China na Ujerumani yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016. Hata hivyo serikali ya Marekani imekuwa ikikwamisha utekelezaji wake licha ya kwamba ilihusika kikamilifu katika kufikiwa mapatano hayo.

Mara kwa mara rais wa Marekani amekuwa akitishia kujitoa kwenye mapatano hayo ambayo yana baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kitendo ambacho kimeufanya ulimwengu usimame kidete kukipinga.