Iran yaulaani vikali utawala wa kijangili wa Israel baada ya vitisho vipya
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umethibitisha utambulisho wake wa kijangili kutokana na sera zake za "kujitanua, uvamizi na ubaguzi" ambazo ni chanzo cha migogoro yote Mashariki ya Kati.
Akihutubu mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alhamisi, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Gholamali Khoshroo amesema: "Kwa hakika, utawala wa Israel ni wa kijangili kwa maana yake halisi-ni ukweli usiopingika kwa jamii ya kimataifa-, kuwa ujenzi wa vitongoji haramu, ubaguzi wa rangi, mzingiro na mauaji ya mara kwa mara ya umati ni vitendo halali kwa utawala ambao unaojinadi kuwa eti ndio pekee ulio na demokrasia Mashariki ya Kati." Amesema madola machache yanayounga mkono ukaliaji mabavu ardhi za wengine ndiyo pekee yanayouunga mkono utawala dhalimu wa Israel
Khoshroo aidha ameikosoa vikali Marekani na baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kupendelea utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kuuwezesha kuendelea kuvuruga amani katika eneo pasina kuwa na hofu ya kuadhibiwa.
Taarifa hiyo imekuja baada ya utawala haramu wa Israel kutoa vitisho kadhaa vya kijeshi dhidi ya Iran na Syria, vitisho ambavyo vimepuuzwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mapema Alhamisi, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel Avigdor Lieberman alitoa vitisho dhidi ya Iran wakati wa mahojiano yake na mtandao unaomilikiwa na Saudi Arabia wa Elaph na kusema kuwa, "iwapo Iran itaishambulia Tel Aviv basi Israel itaishambulia Tehran."
Kwingineko katika taarifa yake, Khoshroo ameashiria mauaji yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel wakati wa kukandamiza maandamano ya amani na kusema, "Iran inatangaza tena kufungamana na watu wa Palestina."
Tokea Machi 30 utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua Wapalestina zaidi ya 42 ambao wamekuwa wakiandamana kila Ijumaa katika Ukanda wa Ghaza wakitetea haki ya kurejea katika ardhi zao zilizoporwa na utawala ghasibu wa Israel mwaka 1948.