Rahim Safavi: Iran imekwamisha njama na mipango ya Marekani Mashariki ya Kati
Msaidizi na Mshauri mwandamizi wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamuu imekwamisha njama na mipango ya Marekani ya kutaka kuwasha moto na kujikita katika Mashariki ya Kati.
Meja Jenerali Sayyid Yahya Rahim Safavi amesema kuwa, hii leo kumeundwa nguvu za muqawama Iraq, Syria na Yemen na kuongeza kwamba, hii leo utamaduni wa jihadi, muqawama, kusimama kidete, kupigania kujitawala na kukabiliana na dhulma na Uistikbari ni mambo ambayo yanapatikana miongoni mwa Waislamu hususan wa eneo la Mashariki ya Kati.
Msaidizi na Mshauri mwandamizi wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwepo wa Wamarekani huko Iraq na Afghanistan haukuwa na kitu kingine ghairi ya uvamizi na vita na Wamarekani wenyewe wamekiri mara kadhaa kwamba, walianzisha kundi la Daesh na ndio walioishajiisha Saudi Arabia pia ili iishambulie kijeshi Yemen.
Kamanda Yahya Rahim Safavi amesema pia kuwa, baada ya kuangamizwa kundi la Daesh huko Iraq na Syria, hivi sasa Wamarekani wanataka kulihamishia kundi hilo nchini Afghanistan.
Aidha amesema bayana kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa muqawama Mashariki ya Kati wameikwaza na kuikwamisha Marekani na kuifanya ishindwe kuunda Mashariki ya Kati mpya na hivyo kulazimika kuondoka huko Syria.
Amesema kuwa, mustakbali wa Mashariki ya Kati umo mikononi mwa mataifa ya eneo hili, na Marekani haina nafasi yoyote.