Iran yaiandikia barua UN kuilaani Israel kwa kuunga mkono magaidi
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa umoja huo na kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwaunga mkono magaidi katika nchi za eneo hili ikiwemo Syria.
Gholamali Khoshroo jana Ijumaa alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, na kusema: Kuna ushahidi wa kutosha kabisa wa kuthibitisha kuwa Israel inayaunga mkono magenge ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika barua yake hiyo, Khoshroo amegusia pia matukio ya tarehe 10 Februari na kusema, siku hiyo, mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa Syria ilitungua ndege ya Israel aina ya F-16 karibu na al Jalil, huko Golan. Utawala wa Kizayuni unadai kuwa ulifanya shambulizi hilo ndani ya ardhi ya Syria baada ya eti ndege isiyo na rubani ya Iran kuingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemweleza Katibu Mkuu wa umoja huo katika barua yake hiyo kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya uchokozi wa mara kwa mara, na Iran ina haki za kujilinda kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa. Hivyo inalitaka Baraza la Usalama la umoja huo lilaani uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni wa Israel na liulazimishe kuachana na chokochoko zake kwani zinahatarisha usalama na amani ya eneo hili zima.
Vile vile amegusia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika ardhi ya Syria na kusema, mashambulizi hayo ni ushahidi wa kutosha wa uchokozi wa Israel kwa nchi hiyo ya Kiarabu na ambao ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.