Rafsanjani: Iran itatoa jibu kali kwa shambulizi lolote dhidi yake
Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran ameonya kuwa shambulizi lolote la kigaidi dhidi ya taifa hili litapokea jibu kali.
Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani amesema vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu vimejiandaa vya kutosha kujibu chokochoko za maadui na kwamba Iran itatoa jibu kali kwa hujuma yoyote ya kigaidi dhidi yake.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Press TV ya Iran, Ayatullah Rafsanjani amesisitizia juu ya udharura wa kupambana na harakati za kigaidi na kuongeza kuwa jambo hilo ni la kibinadamu.
Kwengineko katika maongezi yake, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran ameashiria mbinu inayotumiwa na magaidi ya kuleta mpasuko katika ulimwengu wa Kiislamu kwa misingi ya madhehebu na kuwataka Waislamu kuwa macho kutokana na njama hizo alizozitaja kuwa hatari na haswa kwa eneo hili.
Kadhalika Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani amewataka viongozi wa nchi mbali mbali duniani na jamii ya kimataifa kwa ujumla kushirikiana na kuwasilisha mikakati ya pamoja ya kuyatokomeza makundi ya kigaidi.