Maendeleo yamepatikana katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na Ulaya
(last modified Mon, 28 May 2018 07:26:13 GMT )
May 28, 2018 07:26 UTC
  • Maendeleo yamepatikana katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na Ulaya

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kumepatikana maendeleo mazuri katika mazungumzo baina ya Iran na nchi za Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, lakini bado matoeko yanayofaa hayajapatikana.

Sayyed Abbas Araqchi ameyasema hayo katika mahojiano na Kanali ya Pili ya Televisheni ya Iran na kuongeza kuwa bado Iran haijapata hakikisho kuwa nchi za Ulaya zinaweza kudhamini matakwa yake kikamilifu katika mapatano ya JCPOA.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema mchakato wa mazungumzo unalenga kuhakikisha masharti yaliyowekwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yanafikiwa. 

Inafaa kukumbusha pia kuwa mnamo siku ya Jumatano iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku ya Ijumaa Araqchi alikuwa mjini Vienna Austria kuhudhuria kuanza kikao cha Tume ya Pamoja ya JCPOA ambayo inajumuisha Iran pamoja na Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Umoja wa Ulaya. Kikao hicho kiliitishwa na Iran baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano hayo ya nyuklia ambayo serikali iliyotangulia ya Marekani ilikuwa imeyaidhinisha. Huku akikariri matamshi yasiyo na msingi ya chuki dhidi ya Iran, Trump alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.

Araqchi pia akijibu swali iwapo katika mazungumzo ya Vienna kulifanyika mazungumzo kuhusu uwezo wa makombora ya Iran alisema: "Huo ni mstari mwekundu wa timu ya mazungumzo ya Iran." Amesema, mazungumzo kuhusu makombora hayakufanyika.

Tags