Wendey Sherman akiri: Iran ina utamaduni wa muqawama na inajivunia
Naibu wa zamani wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amekiri kuwa Wairani wana utamaduni wa muqawama na ambao wanajivunia na kujifakharisha nao.
Wendy Sherman, ambaye alikuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani na mjumbe mwandamizi wa ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA ameiambia kanali ya televisheni ya France 24 kuwa baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran, ambayo ina utamaduni wa muqawama na ambao inajivunia na kujifakharisha nao haitorudi kwenye mazungumzo ya rais Donald Trump.
Bi Sherman amesema, John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa serikali ya Marekani na Donald Trump wanatumai kwamba kwa kuiwekea Iran vikwazo vikubwa na vikali zaidi wataweza kuuangusha utawala nchini Iran, lakini siasa hizo dhidi ya Tehran hazina tija kwa sababu vikwazo hivyo vitawafanya Wairani wawe wamoja zaidi.

Mbali na kuielezea kuwa "ghalati na kosa kubwa" hatua ya Washington ya kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA, mjumbe huyo mwandamizi wa timu ya Marekani katika mazungumzo ya nyuklia amekosoa vikali misimamo ya serikali ya sasa ya Washington dhidi ya makubaliano hayo na kumuonya rais wa nchi hiyo na timu yake ya usalama wa taifa juu ya matokeo hasi yatakayosababishwa na misimamo yao hiyo.
Siku ya Ijumaa iliyopita, Michael McFaul, msaidizi wa rais wa zamani wa Marekani Barack Obama naye pia alieleza katika makala iliyochapishwa na gazeti la Washington Post kuwa kujitoa Marekani kwenye JCPOA na kuainishwa masharti 12 na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo kwa ajili ya kufanya mazungumzo mapya na Iran kumeipandisha chati nafasi ya Iran kimataifa na wakati huohuo kuifanya Marekani itengwe.../