Wananchi wa Iran wasisitiza kuhusu kukombolewa Quds Tukufu
Wananchi wa Iran walioshiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds wametoa taarifa na kusisitiza kuhusu kukombolewa Quds (Jerusalem) Tukufu na kujikomboa Wapalestina wanaodhulumiwa kutoka katika makucha ya utawala ghasibu wa Israel.
Aidha wameitaja Israel kuwa donda sugu la saratani ambalo, kwa mujibu wa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, linapaswa kuondolewa.
Washiriki wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran wameitaja kuwa kinyume cha sheria hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu na kuutangaza mji huo kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Waandamanaji wamesisitiza kuwa: "Ukombozi wa Quds na kuunga mkono wananchi Waislamu wanaokandamizwa Palestina ni kipaumbele cha kwanza cha ulimwengu wa Kiisalmu na hatua yoyote yenye lengo la kuondoa kipaumbele hicho na kupotosha fikra za umma wa Kiislamu inalaaniwa vikali."
Aidha washiriki wa maandamano hayo wameashiria njama chafu ya 'Mapatano ya Karne" na kusema njia pekee ya kutatua kadhia ya Palestina ni kuwaruhusu wakimbizi Wapalestina kurejea katika ardhi zao za jadi na kufanyika kura ya maoni huru ili kufikia stratijia ya 'Bahari Hadi Mto". Wamesema suluhu nyingine ghairi ya hiyo itakuwa ni kukanyaga haki za Wapalestina na pia ni uhaini wenye lengo la kuupa uhai utawala unaotenda jinai na bandia wa Kizayuni.
Washiriki wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran wamesema: "Inatazamiwa kuwa Maulmaa na taasisi za Kiislamu katika nchi za Kiislamu zitachukua hatua za kufichua njama mpya za Marekani na utawala wa Kizayuni pamoja na waungaji mkono wao katika eneo na nje ya eneo." Aidha wametaka kufichuliwa njama za baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu ambao wanataka kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu.
Hali kadhalika taarifa hiyo imesema kuangamizwa kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS na magaidi wengine Iraq na Syria, kufeli Saudia katika vita vyake dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Yemen na Bahrain, pamoja na kuwa Riyadh imepata uungajii mkono wa Wazayuni na Wamarekani katika vita hivyo, ni ushindi wa harakati za mapambano ya Kiislamu. Aidha wamesema hawataruhusu maadui wa Uislamu waibue mifarakano baina ya Waislamu kwa lengo la kudhoofisha umma wa Kiislamu kwa maslahi ya utawlaa wa Kizayuni unaokalia Quds kwa mabavu.