Rouhani: Wairani hawawezi kupigishwa magoti na njama za Marekani
Rais Hassan Rouhani amesema katu taifa la Iran haliwezi kupigishwa magoti na njama na mashinikizo ya dola la kibeberu la Marekani.
Rais Rouhani ameyasema hayo katika mkutano wake na wakuu wa Shirika la Utangazaji la Iran IRIB hapa mjini Tehran ambapo ameashiria juu ya uadui wa Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, "Wananchi wa Iran katika hali yoyote ile hawawezi kusalimu amri mbele ya njama na mashinikizo ya watawala wa Washington."
Amesisitiza kuwa, jambo ambalo limeifanya Marekani kushadidisha uhasama wake dhidi ya Iran ni kuliona taifa hili likiendelea kustawi na kufanikiwa katika nyuga mbalimbali za kimataifa, licha ya mashinikizo yake batili ya karibu miongo minne sasa.
Rais Hassan Rouhani amesema Washington imehamakishwa mno na mafanikio makubwa ya Iran katika kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) sanjari na uungaji mkono usio na kikomo wa taifa hili kwa wananchi madhulumu wa Palestina.
Sio vibaya kuashiria hapa kuwa, mwezi uliopita wa Mei, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitoa hotuba isiyo na msingi, ambapo alitaja masharti 12 ambayo Washigton inataka Iran iyatekeleze iwapo inataka kuondolewa vikwazo vya kidhalimu.
Pompeo alitoa hotuba hiyo ya kichekesho siku chache baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuiondoa Marekani kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na kurejesha vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran.