Rouhani: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imevuka njama za adui
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia njama zinazofanywa na Marekani dhidi ya Iran tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kkusema kuwa, taifa na mfumo wa Iran umevuka njama za adui katika vipindi mbalimbali kutokana na kuwa macho na makini.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran na kuongeza kuwa, ubeberu wa kimataifa na uzayuni unakutambua kuwepo Iran ya Kiislamu yenye nguvu na uwezo mkubwa kuwa ni tishio kubwa kwa malengo yake. Amesema kuwa, mara zote taifa la Iran linapopata ushindi mkubwa kikanda na kimataifa, maadui husimama mbele ya taifa hili kutokana na uwezo wa taifa la Iran na taathira yake kubwa.
Amesema katika kipindi cha miaka mingi iliyopita taifa la Iran limestahamili misukosuko mingi na kusimama midete mbele ya mashinikizo ya maadui wake. Ameongeza kuwa: Tangu baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani imefanya vitimbi vingi na kukiuka majukumu yake kwa shabaha ya kutaka kuilazimisha Iran ijiondoe katika makubaliano hayo, lakini imefeli pia katika njama hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi nyingi duniani zinakutambua kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni kinyume na sheria na kukanyaga azimio la Baraza la Usalama na maamuzi ya kimataifa. Ameongeza kuwa, utendaji mzuri wa Iran umewalazimisha Wamarekani kujiondoa katika makubaliano hayo tena kwa kulipa gharama kubwa.
Amesisitiza kuwa, Wairani hawatasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na wataendelea kutetea uhuru na matukufu yao.