Kupinga nchi za Magharibio azimio la kuondolewa vikwazo Iran
Nchi za Magharibi zimezuia kupitishwa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopendekezwa na Korea Kusini kuhusu kuongezwa muda wa kuondolewa vikwazo vya nyuklia Iran.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa Septemba 19 lilichukua uamuzi wa kuitisha kikao maalumu kuhusu kurefushwa muda wa kuiondolea Iran vikwazo. Azimio lililopendekezwa na Korea ya Kusini na kuungwa mkono na China, Russia, Pakistan na Algeria halikupasishwa baada ya kukosa kura zilizohitajika kutokana na upinzani wa nchi za Ulaya na Marekani na kuna uwezekano mkubwa wa kurejeshwa vikwazo na kushtadi mivutano katika eneo.
Azimio hilo lilipigiwa kura nne za ndio na kuungwa mkono Russia, China, Pakistan na Algeria, na nchi za Ulaya ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinazounda kundi la (E3) pamoja na Marekani, Japan na nchi nyingine kadhaa zilipiga kura ya hapana. Guyana na Korea Kusini pia zilijizuia kulipigia kura azimio hilo. Matokeo haya yanamaanisha kumalizika muda wa mwisho wa kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran ambavyo viliwekwa katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA).
Licha ya nchi tatu za Ulaya kuzuia kupasishwa azimio lililopendekezwa na Korea ya Kusini, lakini utaratibu wa "Snapback" hautaanza kutekelezwa papo kwa hapo bali hatua hii itakuwa kwa ajili ya kuishinikiza zaidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikubali matakwa ya Marekani na nchi tatu za Ulaya ndani ya kipindi cha siku 30 zilizosalia hadi kufikia siku ya mwisho ya tarehe 27 Septemba mwaka huu.
Nchi za Ulaya na Marekani zinadai kuwa Iran imekiuka ahadi zake ikiwemo kuzidisha akiba yake ya urani iliyorutubishwa na shughuli za nyuklia zimepindukia mipaka ya makubaliano ya JCPOA hivyo zinashinikiza kurejeshewa vikwazo Iran. Kwa kustafidi na utaratibu huo wa Snapnach, nchi za Ulaya zinafanya kila ziwezalo kwa mara nyingine tena kurejesha vikwazo dhidi ya Iran na zilidai kuwa hatua hii ni ya kisheria katika fremu ya sheria za kimataifa na makubaliano ya JCPOA. Hii ni katika hali ambayo baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya JCPOA mwezi Mei 2018; nchi tatu za Ulaya kwa jina la Troika ya Ulaya na Umoja wa Ulaya hazikuchukua hatua yoyote athirifu ya kuyalinda makubaliano hayo na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa JCPOA na sasa nchi hizo zinataka kutekelezwa utaratibu huo wa kichochezi chini ya mwavuli wa madai yao hayo.
Russia na China zimepinga hatua hii, na kusema kuwa inakinzana na mwenendo wa diplomasia na kutangaza kuwa kurejesha vikwazo kutazidisha tu mivutano katika eneo hili. Nchi mbili hizi zimetangaza rasmi katika taarifa yao ya pamoja kwamba kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ni kinyume cha sheria na ni batili, na hazitaunga mkono vikwazo hivyo bali zitaendelea kushirikiana na Iran. Russia imetangaza kuwa haitambui kivyovyote vile kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran na imetaka kurefushwa kwa miezi sita muda wa kuiondolea Iran vikwazo.
Wakati huo huo weledi wa mambo wanasema kuwa kushindwa kupasishwa azimio la kuongeza muda wa kuiondolea Iran vikwazo kunadhihirisha mgawanyiko mkubwa uliopo katika ngazi ya kimataifa kati ya madola ya Mashariki na Magharibi mwa dunia kuhusu namna ya kuamiliana na miradi ya nyuklia ya Iran; pengo ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwa amani na utulivu wa kikanda na kimataifa.
Amir Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema katika Baraza la Usalama nchi tatu za Ulaya kupinga azimio la kuendelea kuiondolea Iran vikwazo kwamba: Kura ya mgawanyiko imedhihirisha kwamba hakuna muafaka wala kauli moja ndani ya baraza hilo.