Rouhani: Taifa la Iran litaipiga mweleka Marekani katika mapambano ya kusimama kidete
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana jioni alisisitiza kuwa taifa la Iran kamwe haliwezi kuwapigia magoti wavamizi na mabeberu na kuongeza kuwa, Wairani wataishinda Marekani katika mapambano ya maamuzi na ya kusimama kidete.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo katika kikao na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Iran na huku akigusia hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA amesema, katika kipindi cha siku 51 zilizopita za tangu Marekani kujitoa katika mapatano hayo, nchi zote duniani zinaendelea kumlaani Trump na viongozi wa Marekani, lakini hakuna yeyote aliyeweza kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelegeza kamba au imeogopa; bali wote wanalisifu taifa kubwa la Iran kwa busara na hekima zake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, mapatano ya nyuklia ya JCPOA bado yapo na kuongeza kuwa, Wamarekani, Wazayuni na wote wanaoitakia mabaya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili, walidhani kuwa kwa kutangaza Marekani kujitoa kwenye mapatano hayo, Iran nayo ingelijitoa masaa machache tu baadaye, lakini Tehran haikuchukua maamuzi kwa hamaki na pupa.
Aidha amesema, wakati Jamhuri ya Kiislamu ilipotangaza kuwa inatoa fursa kwa ombi la marafiki zake, nchi za Ulaya, Russia na China zilizoiomba Tehran ibakie kwenye mapatano hayo, Wamarekani, Wazayuni na wote wasioitakia mema Iran walipigwa na bumbuwazi, na hapo ndipo walipopata pigo ambalo hawakulifikiria kabisa kutokana na tadibiri ya taifa la Iran.
Vile vile amesema, hapa pana njia tatu. Ya kwanza ni kuipigia magoti Marekani, ya pili ni kusimama kidete kukabiliana nayo sambamba na mivutano ya ndani na ya tatu ni kusimama kidete kukabiliana na Marekani bila ya mivutano ya ndani. Amesema, taifa la Iran limechagua njia hiyo ya tatu na Marekani itakula mweleka katika vita hivyo vya kusimama imara taifa la Iran.