Kuzuia usafirishaji mafuta ya Iran; kutoka matamshi mpaka utekelezaji kivitendo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46684-kuzuia_usafirishaji_mafuta_ya_iran_kutoka_matamshi_mpaka_utekelezaji_kivitendo
Mjadala wa kuyawekea vikwazo mafuta ya Iran na kuzuia kabisa usafirishwaji na uuzaji nje wa bidhaa hiyo ya Iran umezingatiwa na vituo vya utafiti ambavyo vimetahadharisha kwamba, hatua hiyo itapelekea kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo na kufikia hadi dola 150 kwa pipa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2018 08:00 UTC
  • Kuzuia usafirishaji mafuta ya Iran; kutoka matamshi mpaka utekelezaji kivitendo

Mjadala wa kuyawekea vikwazo mafuta ya Iran na kuzuia kabisa usafirishwaji na uuzaji nje wa bidhaa hiyo ya Iran umezingatiwa na vituo vya utafiti ambavyo vimetahadharisha kwamba, hatua hiyo itapelekea kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo na kufikia hadi dola 150 kwa pipa.

Rais Donald Trump wa Marekani akiwa na lengo la kuzuia kabisa hadi kufikia Novemba mwaka huu kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi mafuta ya Iran ameingia uwanjani ili kutimiza lengo hilo. Kwa kuanzia alifanya mazungumzo na Mfalme Salman bin Abdul Aziz Aal-Saud wa Saudi Arabia na baadaye akatuma ujumbe wa Marekani huko Ulaya na mashariki mwa Asia kwa shabaha ya kuwashawishi viongozi husika wasitishe kununua mafuta ya Iran. Hata hivyo kwa sasa swali linaloulizwa na wengi ni kuwa, hivi hizi siasa za kutoa amri na za upande mmoja za Marekani zinaweza kumuondoa katika soko la mafuta duniani mzalishaji muhimu wa mafuta na mwenye nguvu kama Iran? au hata kama hilo litatekelezwa je, matokeo yake mabaya yanaweza kudhibitiwa?

Hotuba iliyokuwa na maana makhsusi ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na njama za Marekani za kuzuia uzaji nje wa mafuta ya Iran ilikuwa jibu zuri na mwafaka kwa swali hilo. Rais Rouhani alisema, njia aliyoichagua Donald Trump ya kuiwekea vikwazo nishati ya mafuta ya Iran haifai na kwa kutumia siasa za kutoa amri haiwezekani kuainisha mwelekeo wa kisiasa katika zama hizi za mfumo wa pande na kambi kadhaa.

Rais Hassan Rouhani

Akihutubia Jumatatu ya wiki iliyopita katika mkutano wa hadhara wa Wairani wanaoishi nchini Uswisi, Rais Hassan Rouhani alisema: "Mmarekani mmoja amesema wanataka kuhakikisha kwamba Iran haiwezi tena kuuza mafuta nje ya nchi na kimsingi inaonekana kuwa hawezi kuchambua maana ya matamshi yake haya

Rais Rouhani alisisitiza kwamba: Hivi kweli inawezekana mafuta ya Iran yasisafirishwe na kuuzwa nje, lakini mafuta ya nchi nyingine za eneo hili yauzwe nje? Mmarekani huyu hajui maana ya maneno haya na anasema, sitaruhusu Iran iuze tone la mafuta nje ya nchi. Kama unaweza basi fanya na utaona matokeo yake". 

Nafasi ya kiistratejia ya Iran, masoko tofauti ya kuuza mafuta ya Iran na muhimu kuliko yote, kupendwa mafuta ya Iran ni mambo ambayo kivitendo yanakwamisha kufutwa katika soko la mafuta nchi kama Iran. Kwa hakika kuzuia kuuzwa nje mafuta ya Iran ni katika fremu ya siasa za Trump za "Yote au Kuambulia Patupu" ambazo ni ndoto za alinacha. Ndoto hizo za alinacha za Marekani zinazoshuhudiwa kikamilifu katika mwenendo wa nchi hiyo na Saudi Arabia.

Rais Donald Trump wa Marekani

"Ongeza uzalishaji mafuta, kwani kwa hizi pesa ndogo ninazopata kutoka kwako, nimeweza kukulinda na kudhamini usalama wako"; maneno haya ni mithili ya kuikamua Saudia na kuwadhalilisha Wasaudia. Fauka ya hayo, kivitendo Saudia haina uwezo wa kufidia pengo litakalotokana na vikwazo vya mafuta ya Iran. Kwa hakika Saudia inaweza kwa taabu mno kuzalisha mapipa milioni 11 kwa siku katika mwaka huu.

Gerry Russell mtaalamu wa taasisi ya S&P Global Platts  anaamini kwamba: Kuzalisha mapipa milioni 11 kwa siku maana yake ni kuushinikiza kupita kiasi mfumo wa mafuta wa Saudia. Kanali ya habari ya Bloomberg ilitangaza pia Jumapili iliyopita kwamba, wakati vikwazo dhidi ya Iran vitakapotekelezwa mwezi Novemba mwaka huu, wazalishaji wa mafuta hawatakuwa na uwezo wa kutosha wa kufidia pengo la mafuta ya Iran. Endapo Trump atafanikiwa kusimamisha kikamilifu mafuta ya Iran, wazalishaji wa mafuta watapaswa kufidia kila siku mapipa milioni 2.7 ya mafuta ya Iran. Hili ni shimo kubwa ambalo kulijaza ni kibarua kigumu.

Kuyawekea vikwazo kikamilifu mafuta ya Iran ni tumaini la Trump ambalo ana kibarua kigumu kulifikia na hata Saudia yenyewe haina ubavu wa kitaalamu na kielimu wa kutekeleza takwa hilo la Rais wa Marekani. Kuzuia kuuzwa nje mafuta ya Iran hasa kwa kuzingatia ukweli wa mambo ulivyo hivi sasa katika soko la mafuta duniani, si kwa maslahi ya walimwengu, na bila shaka chokochoko hizi za Trump zitaufikisha ulimwengu katika mshtuko mbaya wa mafuta.

Rais wa Marekani amechagua kipindi kibaya mno na bila shaka kumuondoa mzalishaji mkubwa kama Iran katika mzunguko wa mafuta ni jambo ambalo halitapita hivi hivi bila ya kuwa na matokeo mabaya.