Kiongozi Muadhamu: Ndoto potovu ya kuyahudisha Palestina na 'Muamala wa Karne' haitatimia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama chafu ya Marekani na Utawala wa Kizayuni inayojulikana kama 'Muamala wa Karne' dhidi ya Palestina na Quds Tukufu na kusema: "Uyahudishaji Palestina ni ndoto potovu ambayo haitatimia"
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo katika mkutano jana Jumapili na kuongeza kuwa, ndoto hiyo ya kuyahudisha Palestina na 'Muamala wa Karne' vyote havitekelezeki.
Alhamisi iliyopita Bunge la Utawala wa Kizayuni wa Israel lilipasisha sheria ya 'Nchi ya Kiyahudi. Sheria hiyo ya kibaguzi imewapokonya Waislamu na Wakristo Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) haki ya kuainisha mustakbali wao na haki hiyo imepewa Mahayudi pekee.
Sheria hiyo imelaaniwa vikali kimataifa lakini utawala wa Kizayuni wa Israel umeonyesha kutojali na unaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa lengo la kuyahudisha Quds Tukufu na ardhi zote za Wapalestina.
Sambamba na njama hiyo, Marekani inafuatilia mpango wa kuzilazimu nchi za Kiarabu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel katika fremu ya nara na kauli mbiu ya 'Muamala wa Karne' kwa lengo la kuimarisha mpango huo wa kuyahudisha ardhi za Palestina.