Rais Rouhani: Maadui wanafuatilia vita vya kisaikolojia na kiuchumi dhidi ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanafuatilia vita vya kisaikolojia na kiuchumi dhidi ya mfumo na watu wa Iran.
Rais Rouhani aliyasema hayo mjini Tehran jana Alasiri katika kikao cha Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni ambapo ameashiria vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya taifa la Iran na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuinua kiwango cha ufahamu, matumaini na ushiriki wa wananchi, inaweza kupita kipindi hiki kwa kasi na gharama ndogo."
Rais Rouhani ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo amekumbusha kuhusu utamaduni wa kidini wa taifa la Iran na kusema: "Taifa la Iran litapata kinga mbele ya hujuma ya tamaduni mbali mbali hasa utamaduni wa madola ya Magharibi.
Rais wa Iran aidha ametuma salamu za pongezi na fanaka kwa taifa kwa munasaba wa 'Wiki ya Serikali' na kusema: "Serikali ni sehemu ya kuwahudumia wananchi na katika kipindi hiki serikali itafanya kila iwezalo kufuata nyayo za mashahidi Rajai na Bahonar katika kutekeleza majukumu yake ya kimapinduzi na kitaifa kwa njia sahihi.
Itakumbukwa kuwa Agosti 30 mwaka 1981 Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilitekelezwa na Kundi la Kigaidi la Munafiqeen (MKO).
Katika kuwaenzi mashahidi hao baina ya Agosti 24 na 30 huadhimishwa kote Iran kama 'Wiki ya Serikali.